ISIKUPITE

Blogroll

Friday, 5 October 2018

MBIO ZA BAISKELI KUZINDULIWA LEO


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, leo anatarajiwa kuzindua rasmi mashindano ya mbio za baiskeli yenye lengo la kukusanya zaidi ya Sh. milioni 340 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Mashindano hayo ambayo yatazinduliwa jijini Dar es Salaam yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mashindano hayo yameandaliwa na kampuni ya uchimbaji wa madini Tanzania ya ACACIA kwa kushirikiana na taasisi binafsi kutoka Canada ‘CanEducate’ na yanalenga kukusanya fedha za kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kumudu gharama za shule hasa watoto wa kike wanaotoka katika familia duni zinazozunguka migodi ya kampuni hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo nchini, Asa Mwaipopo, Meneja Uboreshaji tija kutoka ACACIA, Janeth Reuben, alisema mashindano hayo wameyapatia jina la ‘Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge’ na yanaenda sambamba na mpango wa kampuni wa kujenga jamii endelevu.

Alisema mpango huo unaofahamika kwa jina la CanEducate, unatoa kipaumbele katika kuhakikisha hasa watoto wa kike - wanapata elimu bora kama njia mojawapo ya kujikwamua na umaskini na kufanikisha dhamira ya serikali ya kuinua uchumi.

Alisema hadi sasa mpango huo wa CanEducate ulioanza mwaka 2011, umetumia kiasi cha Sh. milioni 494 kwa kuwadhamini wanafunzi 3936, na kuziwezesha kwa njia mbalimbali shule zaidi ya tisa.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Baiskeli Tanzania (Chabata), Godfrey Mhagama, alisema tangu mwaka 2014 Acacia imewasaidia kuboresha mchezo huo kwa kuwapatia vifaa mbalimbali muhimu vya usalama na misaada mingine katika chama.

No comments:

Post a Comment